Jumapili 4 Oktoba 2026 - 18:10
Mufti wa Uganda Aunda Kamati ya Kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa Lugha ya Langi

Hawza/ Mufti wa Uganda, Sheikh Shaban Ramadhan Mubaje, ameunda kamati ya wajumbe saba inayowakilishwa na wanazuoni wa Kiislamu na wataalamu wa lugha, yenye jukumu la kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa lugha ya Langi, moja ya lugha za asili zinazozungumzwa kwa wingi kaskazini mwa Uganda.

Kwa mujibu wa sirika la habari la hawza, wawakilishi wa kamati hiyo ni Sheikh Sadick Ayo, Imamu wa Msikiti wa Idi Amin katika Jiji la Lira; Sheikh Shaban Sadam Nasser, Imamu wa Msikiti wa Taqwa; Sheikh Hafiz Nurain Maganda, mwenye shahada ya uzamili katika Sheria na Mkurugenzi wa Shule ya Awali na Msingi ya Kiislamu ya Haif mjini Lira; Bw. Ocom Ismael, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Harvard; Bw. Ogal Ismael, mshauri na mtafsiri wa vifaa vya kujifunzia kwa lugha ya Langi katika Wizara ya Elimu na Michezo; Sheikh Ali Yakub Okwir, Kadhi wa Wilaya; na Sheikh Abdul-Karim Omar, Naibu Kadhi.

Kamati hiyo imekubali kutekeleza jukumu lililoelezwa kuwa la kihistoria, la kuifanya Qur’ani Tukufu ipatikane kwa urahisi kwa Waislamu wanaozungumza Langi kupitia tarjama katika lugha yao mama. Uzinduzi huo ulikuwa sehemu ya shughuli zilizoandaliwa kuadhimisha kuzaliwa Mtume Muhammad (saww), na ulifadhiliwa na Haj Masoud Obeid, mfanyabiashara mashuhuri wa Kampala na mzawa wa eneo hilo.

Mufti Mubaje alisafiri kutoka Zombo katika Kanda ya West Nile Ijumaa alasiri na kuwasili katika Jiji la Lira usiku wa siku hiyo, huku akiandamana na viongozi wakuu wa Baraza Kuu la Waislamu Uganda [UMSC]. 

Alipowasili, ujumbe huo ulipokelewa na wenyeji pamoja na viongozi wa Kiislamu kutoka eneo hilo. Siku iliyofuata, Jumamosi 3 Oktoba 2026 (11 Mehr 1405), Mufti na ujumbe wake waliwasili katika eneo la hafla, ambako walipokelewa na viongozi wa Kiislamu wakiongozwa na Sheikh Musa Khelili, Msaidizi wa Kikanda wa Mufti kwa Kanda ya Kaskazini, pamoja na Mamakadhi wa wilaya za Kiislamu jirani. Maadhimisho hayo yalipambwa na maonyesho ya vikundi vitatu vya kaswida za Kiislamu—Kampala Mataali Events, West Nile Mataali Group na Lango Mataali Group—vilivyowaburudisha washiriki kwa nyimbo za kumsifu Mtume Muhammad (saww).

Baadaye, hotuba zilitolewa na viongozi kadhaa wa Kiislamu na wageni, akiwemo Mheshimiwa Asuma Wasema, Mheshimiwa Omar Kanjule na Mheshimiwa Hajjat Aisha Abdu, mwakilishi wa Baraza la Waislamu la Uganda (UMSC) kutoka wilaya za Kiislamu za Lango na Apac.

Sheikh Khelili, kupitia Katibu wake wa Kanda, Bw. Odongo Edris, aliwasilisha ripoti ya kurasa nne kuhusu hali ya jamii ya Waislamu katika Lango. Ripoti hiyo ilihusu masuala ya utawala na uongozi, pamoja na usimamizi wa mali za Waislamu katika Wilaya ya Kiislamu ya Lango.

Kwa upande mwingine, Mheshimiwa Aluma aliwafikishia washiriki taarifa kuhusu maendeleo katika makao makuu ya Baraza la Waislamu la Uganda (UMSC), ikiwemo maandalizi ya Kongamano lijalo la Kitaifa la Vijana Waislamu, lililopangwa kufanyika mwishoni mwa Oktoba na linatarajiwa kufunguliwa na Rais Yoweri Museveni. Aliwataka vijana Waislamu kutoka kaskazini mwa Uganda kujitokeza kwa wingi kushiriki katika kongamano hilo.

Dkt. Sheikh Bukenya na Haj Masoud Obeid pia walihutubia mkutano huo kabla ya Mufti kutoa hotuba kuu.
Akizungumza kwa Kiswahili na Kiingereza, Mufti Mubaje alikumbusha hali za kidini na kijamii zilizokuwepo kabla ya kuzaliwa Mtume Muhammad (saww), huku akielezea kipindi hicho kuwa kilitawaliwa na ujinga mkubwa, ibada za masanamu na umwagaji wa damu. Alisema kuja kwa Mtume Muhammad ilikuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa kwa wanadamu, kwani Mwenyezi Mungu alimtuma kama rehema kwa walimwengu.

Mufti aliwataka Waislamu kushikamana na mafundisho ya Mtume kuhusu udugu, heshima na kuishi kwa amani, huku akisema kuwa maadili hayo ni muhimu kwa mafanikio duniani na akhera.

Pia alisema kuwa uamuzi wa kuadhimisha kila mwaka mazazi ya Mtume Muhammad katika ulimwengu wa Kiislamu ulifikiwa kupitia Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu [OIC], ambayo Uganda ni mwanachama wake.

Mufti Mubaje alimshukuru Haj Masoud Obeid kwa kuandaa maadhimisho hayo katika eneo analotoka, na akawahimiza Waislamu wengine kuiga juhudi zake za kuunga mkono shughuli zinazoiimarisha jamii ya Waislamu.

Baadaye Mufti alitoa zawadi za fedha taslimu na vikombe kwa vikundi vitatu vya kaswida za Kiislamu vilivyoshiriki mashindano ya mwaka [2026]. Kampala Mataali Events kiliibuka mshindi wa jumla, kikifuatiwa na Lango Mataali Group, huku West Nile Mataali Group kikishika nafasi ya tatu.
Maadhimisho hayo yalihitimishwa kwa shukrani kutoka kwa wanawake Waislamu wa Lango, wakiongozwa na mwakilishi wao wa kitaifa.

Chanzo: Baraza Kuu la Waislamu la Uganda (UMSC).

Mufti wa Uganda Aunda Kamati ya Kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa Lugha ya Langi

Mufti wa Uganda Aunda Kamati ya Kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa Lugha ya Langi

Mufti wa Uganda Aunda Kamati ya Kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa Lugha ya Langi

Mufti wa Uganda Aunda Kamati ya Kutarjumu Qur’ani Tukufu kwa Lugha ya Langi

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha